
Jumanne hii bungeni Dodoma palichimbika. Ni baada ya mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, kuwasilisha taarifa akihoji sababu za jeshi la polisi kuwakamata wabunge wa upinzani bila sababu za msingi na ndipo wabunge wa upinzani waliamua kulisusia bunge.
Katika tukio hilo lililotokea jana jioni, wabunge wote wa upinzani walilazimika kutoka nje baada ya kutoridhishwa na majibu ya Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, aliyoyatoa wakati akijibu taarifa hiyo ya Zitto.
Awali, Dk. Tulia alilieleza Bunge jinsi alivyopata ujumbe wa maandishi kutoka kwa Zitto, ukimwomba ampe nafasi ya kutoa taarifa katika suala alilokuwa nalo. Baada ya kukamilisha kauli hiyo, Zitto alisimama na kulieleza Bunge kuwa utaratibu wa Jeshi la Polisi wa kuwakamata wabunge wa upinzani unakiuka taratibu na kanuni za Bunge.
“Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge letu liko katika nchi za Jumuiya ya Madola na linaongozwa na katiba, kanuni, sheria za mabunge mengine, maamuzi ya maspika wengine na sheria zingine. Hivi karibuni, Mbunge wa Arusha, Godbless Lema (Chadema), alikamatwa nje ya Bunge baada ya kuhudhuria vikao vya Bunge na hadi sasa Bunge halina taarifa.
“Kwa mujibu wa kanuni zetu na nchi za Jumuiya ya Madola, polisi wanapotaka kumkamata mbunge, lazima kwanza wampe taarifa Spika wa Bunge na baadaye Spika aliambie Bunge juu ya taarifa hiyo na kueleza ni kwanini mbunge amekamatwa. Pamoja na Lema kuwekwa ndani, Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali amefungwa jela miezi sita na hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kwa Spika wa Bunge na hata Bunge halijaelezwa juu ya tukio hilo,” alisema.
“Katika hayo, Sheria ya Bunge ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge inakiukwa kwa sababu hata jana (juzi), Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), alikamatwa bila Spika kuwa na taarifa. Mimi binafsi nilimpigia simu Spika kumuuliza juu ya tukio hilo, Spika akasema hakuwa na taarifa, hii ni dharau kubwa sana kwa Bunge. Mheshimiwa Naibu Spika, mhimili wa Bunge umedharauliwa mno kwani hata mimi nimepata taarifa, kwamba polisi wananisubiri ili nikitoka nje wanikamate na siogopi kukamatwa.”
“Aliendelea, “Kwahiyo naomba jambo hili lijadiliwe na litolewe uamuzi kwa sababu mwaka 2011, Bunge la Uingereza ililetwa hoja kama hii na Bunge likaijadili na kuitolea uamuzi.”
Akitoa ufafanuzi wa taarifa hiyo, Naibu Spika alivitaja vifungu vya 6, 7, 8, 12 na 13 vya Kanuni ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, vinavyoeleza juu ya mbunge kukamatwa.
“Kwahiyo, kifungu cha 12 kinasema Spika atapewa taarifa pale tu mbunge atakapokuwa akitakiwa kukamatwa kwa makosa ya madai na si kwa makosa yasiyokuwa ya madai. Hivyo basi, taarifa ya mheshimiwa Zitto siwezi kuruhusu ijadiliwe kwa sababu makosa hayo si ya madai,” alisema Naibu Spika.
Baada ya majibu hayo, wabunge wa upinzani walianza kulalamika akiwemo Mbunge wa Serengeti, Marwa Chacha (Chadema), aliyesimama akitaka apewe ruhusa ya kuzungumza. Hata hivyo, Naibu Spika hakumruhusu na alipomtaka akae ili Bunge liendelee, alikataa na hivyo kuagiza askari wa Bunge wamtoe nje kwa nguvu, jambo ambalo lilipingwa na wabunge wa upinzani na kuamua kutoka nje ya Bunge. Wakati huo huo wabunge hao kutoka nje, Zitto aliwaambia wanahabari kwamba wataendelea kusimamia Kanuni za Bunge ili zisivunjwe kama anavyofanya Naibu Spika.
“Lissu amekamatwa bila kujua sababu za kukamatwa kwake na inawezekana mpaka sasa hajajua. Sasa Naibu Spika atuambie ni wakati gani Spika anajua mbunge anapokamatwa, anakamatwa kwa makosa ya madai au ya jinai. Mabunge yote duniani utaratibu ni kwamba unapotaka kumkamata mbunge, lazima utoe notisi kwa Spika, lakini hapa kwetu huo utaratibu haufanyiki. Katika hili, Naibu Spika amekwenda kinyume na ulinzi wa hadhi ya Bunge,” alisema Zitto.
Kwa upande wa Mbunge wa Kawe, Halima Mdee aliwaambia wanahabari, “Hatukubaliani na kilichofanywa na Naibu Spika pamoja na kutoka bungeni leo, kesho tutaingia na kuendelea kudai haki zetu maana hatukubali kuwa tunakamatwa kila wakati,” alisema Mdee.
Post a Comment